MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA YATAJWA KUWA CHANZO KIKUU CHA MAGONJWA YA AKILI POKOT MAGHARIBI.

Idadi kubwa ya visa vya ugonjwa wa akili miongoni mwa vijana husababishwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Haya ni kwa mujibu wa daktari mkuu katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Dkt. Simon Kapchanga ambaye alisema japo kuna vyanzo vingine vya tatizo hilo, asilimia kubwa ya ugonjwa huo hutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha Kapchanga alisema watu ambao wamekuwa wakitumia dawa hizo kwa muda wako katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa akili iwapo wataacha kuzitumia dawa hizo, kutokana na uraibu ambao mara nyingi huwa vigumu kumwondokea mtumizi.

“Tatizo kubwa ambalo linasababisha ugonjwa wa akili ni matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana. Japo kuna visababishi vingine, lakini kuu zaidi ni matumizi ya mihadarati. Pia wakati mwingine mtu ambaye ametumia mihadarati kwa muda, hupatwa na ugonjwa wa akili iwapo atajaribu kuacha matumizi yake kutokana na uraibu.” Alisema Kapchanga.

Alielezea haja ya serikali pamoja na wadau kuweka mikakati itakayosaidia kuzuia matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa mafunzo kuhusu athari za matumizi ya dawa hizo, pamoja na idara za usalama kukaza kamba ili kufanya vigumu kwa dawa hizo kupatikana.

“Kama jamii na kama serikali tunapasa kutilia maanani mbinu za kuzuia matumizi ya mihadarati kwa, mfano kupitia mafunzo kuhusu madhara ya dawa hizo. Pia idara za usalama zinapasa kukaza kamba ili kuhakikisha kwamba dawa hizo hazipatikani kwa urahisi.” Alisema