MATOZO YALIYOPENDEKEZWA KATIKA MSWADA WA KIFEDHA MWAKA 2023/2024 YAENDELEA KUIBUA HISIA KINZANI NCHINI.

Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa nchini kufuatia mapendekezo ya rais William Ruto katika mswada wa fedha wa mwaka 2023/2024 ambapo amependekeza kuongeza viwango vya ushuru unaotozwa kwa wakenya ili kufanikisha miradi mbali mbali ya serikali.

Wa hivi punde kutolea hisia mapendekezo hayo ni naibu gavana kaunti kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole ambaye alimtaka rais Ruto kuahirisha mipango hiyo hadi mwaka ujao hasa pendekezo la asilimia 3 ya mishahara ya wafanyikazi wa umma ambayo analenga kuelekeza kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Komole alisema kwamba wengi wa wafanyikazi wa umma hawapo tayari kwa mabadiliko hayo hasa yanayohusu kukatwa mishahara yao ikizingatiwa hali ngumu wanayopitia wakati huu kufuatia kupanda gharama ya maisha.

“Namsihi rais wetu kwamba aangalie vizuri kuhusu mapendekezo yake hasa swala la kuwatoza wafanyikazi asilimia 3 ya mishahara yao kufanikisha mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu. Ningependelea pendekezo hilo litekelezwe mwaka ujao kwa sababu kwa sasa wakenya hawako tayari kufuatia gharama ya juu ya maisha.” Alisema Komole.

Hata hivyo kauli tofauti na hiyo ilitolewa na mwakilishi wadi ya Kapenguria Richard Mastaluk ambaye aliwataka wakenya kumuunga mkono rais Ruto katika juhudi zake za kuliokoa taifa kutokana na kuporomoka zaidi kiuchumi kwa kukumbatia mapendekezo hayo.

Alisema kwamba hamna taifa ambalo litaweza kuimarika kiuchumi iwapo linatekeleza shughuli zake kwa kutegemea mikopo kutoka mashirika mbali mbali na mataifa ya kigeni.

“Tunafaa kumuunga mkono rais wetu kunusuru uchumi wa nchi kwa kulipa ushuru. Nawarai wakenya wenzangu kwamba kama sisi ni watu tunaojali nchi yetu ni lazima tulipe hiyo asilimia 3 kwa sababu hamna nchi itakayoendelea kwa kutegemea mikopo.” Alisema Mastaluk.