MATAMSHI YA MBUNGE WA EALA KUHUSU KUJIHAMI KWA BUNDUKI WAKAZI WA BARINGO YAIBUA HISIA KALI.


Wakazi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kuelezea gadhabu zao kufuatia video ambayo imeenea mitandaoni ikimwonyesha mbunge katika bunge la Afrika mashariki EALA Florence Jematia akipendekeza wakazi wa kaunti ya baringo kununua bunduki ili kujilinda baada ya serikali kushindwa kuwahakikishia wakazi wa eneo hilo usalama.
Wakiongozwa na Charles Lokwachai wakazi hao wamesema kuwa huenda kauli hii ikachangia kuongezeka zaidi utovu wa usalama katika eneo la bonde la Kerio ambalo tayari limeshuhudia visa vingi vya uvamizi ambavyo vimepelekea maafa ya wakazi wengi.
Wakazi hao aidha wamewashutumu vikali viongozi ambao walikuwa katika mkutano uliotumika na Jematia ambaye pia ametangaza azma ya kuwania wadhifa wa mwakilishi kina mama kaunti ya Baringo kutoa matamshi hayo kwa kutoyashutumu.
Wamezitaka idara za usalama katika kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Baringo kushirikiana na kuhakikisha kuwa hatua inachukuliwa dhidi ya kiongozi huyo kwani huenda yakazidisha mahangaiko yanayowakumba wakazi kufuatia visa vya uvamizi.