MASTALUK: NITAWEKA NGUVU ZANGU ZOTE KWENYE SEKTA YA ELIMU KATIKA HIMAYA YANGU.

Mwakilishi wadi ya Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Richard Mastaluk amesema kwamba atawekeza kikamilifu katika swala la elimu ili kuhakikisha kwamba sekta ya elimu inaimarishwa katika wadi hiyo.

Mastaluk alisema eneo hilo limesalia nyuma kwa muda na lengo lake ni kuhakikisha kwamba wanafikia viwango vya maeneo mengine kielimu ambapo wakazi waliosomea taaluma mbali mbali watapatikana.

Aidha Mastaluk alisema ameandaa kikao na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu ikiwemo wazee wa mitaa katika juhudi za kupanga mikakati ya kuhakikisha kila mtoto eneo hilo anahudhuria masomo kwa manufaa yao ya siku za usoni.

“Nimekutana na wazee wote wa mitaa eneo hili ili kupanga mikakati ya kuboresha elimu katika sehemu hii. Nataka niweke nguvu sana katika sekta ya elimu ili pia tuafikie viwango vya maeneo mengine kwa sababu hii sehemu iliachwa nyuma kwa muda.” Alisema mastaluk.

Alikuwa akizungumza wakati akizindua zoezi la kupeana viti vya shule za chekechea eneo la Chemwochoi, akivitaja kuwa vya hali ya juu na ambavyo vitasambazwa katika shule mbali mbali za eneo hilo.

“Niliona kwamba hawa watoto wa chekechea hawataweza kukalia madawati ya kawaida kwa sababu ni nzito sana kwao. Ikabidi nitafute viti vya plastiki ambavyo ni vya hali ya juu na ambavyo vitadumu kwa miaka mingi.Viti hivi vitasambazwa katika shule mbali mbali za wadi hii ili kutumika na watoto hawa.” Alisema.

[wp_radio_player]