MASOMO YAREJELEWA BAADA YA LIKIZO YA UCHAGUZI.


Shughuli za masomo zinaporejelewa leo baada ya kufungwa shule kwa kipindi cha majuma mawili ili kupisha maandalizi ya uchaguzi mkuu, wazazi wametakiwa kuhakikisha kuwa wanao wanarejea shuleni kwa wakati unaofaa.
Akizungumza na kituo hiki OCS wa kituo cha polisi cha kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi Tom Nyanaro amesema kuwa wanafunzi hasa wa kike eneo hilo wako katika hatari kubwa ya kukatizwa ndoto zao iwapo watasalia nyumbani kwa kipindi kirefu.
“Watoto wasichana wakikaa nyumbani katika eneo hili la Kacheliba pamoja na eneo zima la Pokot kaskazini wako katika hatari ya kuchukuliwa na vijana ambao wanachunga ng’ombe kama wanawake.” Amesema.
Nyanaro aliongeza kwamba, “kwa sababu uchaguzi ulikamilika na watoto wanarejea shuleni, wazazi wawarejeshe wanao wa kike shuleni kwani wakiwa nyumbani kwa muda mrefu si vizuri.”
Nyanaro amesema kuwa usalama wa watoto wa kike umehakikishwa iwapo watakuwa shuleni kuliko wanapokuwa nyumbani.
Hata hivyo Nyanaro amesema kuwa wanaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anapewa fursa ya kuendeleza masomo ili kuafikia ndoto yake maishani sawa tu na wenzao wa kiume.
“Tunaendelea kufuatilia watoto ambao wazazi wao walitaka kuwaoza ila hawakufaulu. Pia tunatoa uhamasisho kwa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa watoto wa kike nafasi ya kusoma ili kuafikia ndoto yao maishani.” Alisema.

[wp_radio_player]