MASOMO YAENDELEA KULEMAZWA CHESOGON LICHA YA HAKIKISHO LA SERIKALI.
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia hatua ya kutofunguliwa baadhi ya shule ambazo ziliathirika na hali ya utovu wa usalama mipakani pa kaunti hiyo, hasa eneo la chesogon licha ya ahadi za serikali kwamba shule hizo zingefunguliwa mwanzoni mwa mwaka huu.
Wakiongozwa na seneta wa kaunti Julius Murgor na mbunge wa sigor Peter Lochakapong, viongozi hao walisema kwamba masomo katika shule hizo yameendelea kulemazwa kutokana na kazi duni ambayo ilitekelezwa na maafisa ambao walipewa jukumu la kukarabati shule hizo.
Viongozi hao walisema licha ya mamilioni ya pesa kutengwa kutekeleza ukarabati wa shule hizo, hamna kazi ya kuridhisha ambayo imefanywa, wakidai huenda fedha hizo zilifujwa na waliopewa jukumu la kutekeleza shughuli hiyo.
“Serikali iliahidi kwamba shughuli za masomo zitarejelewa mwaka huu katika shule zilizoathirika na utovu wa usalama, lakini hadi kufikia sasa hamna masomo katika shule hizo. kazi ambayo imefanywa na waliopewa jukumu la kukarabati shule hizo ni duni sana. Kuna ufisadi mkubwa ambao unaendelezwa katika shughuli hiyo.” Walisema.
Wakati uo huo viongozi hao walimtaka waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kuzuru kaunti za eneo la bonde la kerio na kukutana na viongozi katika eneo hilo, ili kufanya kikao cha pamoja ambacho kitapelekea kupatikana suluhu ya kudumu kwa swala la utovu wa usalama.
“Tunamtaka waziri wa usalama Kithure Kindiki kuja eneo hili na kukutana na viongozi wa kaunti za bonde la kerio ili tupate suluhu ya kudumu kwa tatizo hili la utovu wa usalama, ili kuwe na maendeleo maeneo haya.” Walisema.