MASHIRIKA YASIYO YA SERIKALI YAOMBWA KUWASAIDIA WAATHIRIWA WA MAFURIKO ORTUM.

Mbunge wa Pokot kusini katika kaunti ya Pokot magharibi David Pkosing ametoa wito kwa mashirika mbali mbali yasiyo ya serikali kuingilia kati na kuwasaidia wakazi ambao walipoteza mali yao kufuatia mafuriko makubwa yaliyoshuhudiwa eneo la Ortum.

Akizungumza alipozuru eneo hilo, Pkosing alisema kwamba takriban wafanyibiashara 30 waliathirika na mafuriko hayo ambayo yalisomba vibanda vyao huku baadhi ya maduka yakibomolewa, na kwamba kama mbunge pekee hatoweza kustahimili uzito huo.

“Naomba mashirika yasiyo ya serikali kuingilia kati na kuwasaidia wakazi ambao waliathirika na mafuriko hayo. Mimi siwezi peke yangu ikizingatiwa kiwango cha uharibifu. Ni takriban watu 30 ambao wameathirika katika tukio hilo.” Alisema Pkosing.

Aidha, Pkosing alitoa wito kwa gavana Simon Kachapin kwa ushirikiano na wabunge katika bunge la kaunti hiyo kuharakisha kubuniwa hazina ya kushughulikia majanga ili kugharamia visa kama hivi, akitumia fursa hiyo kusuta uongozi uliotangulia kwa kile alidai kufuja misaada iliyokuwa ikitolewa kwa waathiriwa wa majanga.

“Naomba waakilishi wadi katika kaunti hii kushirikiana na gavana ili kuharakisha kubuniwa hazina ya kushughulikia majanga. Naamini gavana wa sasa anasikiliza watu. Si kama wale wengine ambao walikuwa wanaweka misaada iliyotolewa kwa waathiriwa na hata kufuja misaada yenyewe.” Alisema.

Wafanyabiashara eneo hilo walielezea kuathirika pakubwa wakitoa wito kwa serikali kuweka mikakati ambayo itazuia hali kama hii kushuhudiwa tena hasa wakati huu ambapo mvua inaendelea kushuhudiwa maeneo mbali mbali ya nchi.

“Tumepoteza mali nyingi sana kufuatia mafuriko haya na hasara ambayo tumepata ni kubwa zaidi. Tunaomba serikali lkuweka mikakati ya kukabili majanga kama haya siku za usoni.” Walisema wafanyabiashara.