MASHIRIKA YANAYOPAMBANA NA UKEKETAJI YATAJA UKOSEFU WA UFADHILI KUWA CHANGAMOTO KUU KWA SHUGHULI ZAO.
Mashirika yanayoendeleza vita dhidi ya ukeketaji katika kaunti hii ya Pokot magharibi yametaja ukosefu wa ufadhili wa mashirika hayo kifedha kuwa changamoto kuu katika juhudi zao kuhakikisha kwamba tamaduni hii inatokomozwa miongoni mwa jamii.
Afisa katika wakfu wa Men End FGM foundation Peter Kemei alisema licha ya kwamba vita dhidi ya tamaduni hiyo vimekuwepo kwa zaidi ya miaka 30, vimekosa kuzaa matunda hitajika kutoka mashirika mengi kukosa fedha za kutosha kufanikisha shughuli zake.
Kemei alitoa wito kwa serikali kuu kwa ushirikiano na ya kaunti ya Pokot magharibi kutenga fedha katika bajeti ambazo zitatumika katika kuyafadhili mashirika haya ili kuhakikisha kwamba yanatekeleza majukumu yake inavyopasa na kutokomeza tamaduni hii potovu.
Aidha alitaja ukosefu wa usalama maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo kuwa unaofanya vigumu kwa mashirika hayo kufika maeneo husika kuendeleza uhamasisho dhidi ya ukeketaji.
“Vita dhidi ya ukeketaji katika kaunti hii vimekuwepo kwa zaidi ya miaka 30 ila havijaweza kuafikia malengo hitajika, kwa kuwa mengi ya mashirika ambayo yanaendeleza harakati hizo yanakabilkiwa na changamoto ya kifedha. Ni wakati serikali inapasa kutenga bajeti ili kuyafadhili mashirika haya iwapo tunatarajia vita hivi kufaulu.” Alisema Kemei.
Kauli yake ilisisitizwa na Faith Chepkasi afisa wa shirika hilo ambaye aidha alielezea haja ya vijana kutumia pakubwa mitandao ya kijamii kueneza ujumbe dhidi ya ukeketaji na mimba za mapema ili kuwahamasisha vijana wenzao ambao bado wanashikilia hulka hizo kuziasi.
“Sasa tunaishi katika kizazi cha kidijitali na itakuwa bora iwapo vijana watahusika pakubwa katika vita hivi kwa kueneza jumbe za kuwahamasisha vijana wenzao ambao bado wanashikilia tamaduni hizi kuziasi. Kwa sababu ni kupitia mitandao tu ambapo wengi wa vijana watafikiwa.” Alisema Chepkasi.