MASHIRIKA YA KIJAMII POKOT MAGHARIBI YAELEZEA WASI WASI KUHUSU VIWANGO VYA DHULUMA DHIDI YA WANAWAKE.
Mashirika mbali mbali ya kijamii katika kaunti ya Pokot magharibi yalitumia hafla ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake duniani jumatano kuwahamsasisha wanawake kuhusu haki zao katika jamii.
Wakiongozwa na Salome Cheruto na Faith Chepkasi ambao waliwakilisha Wakfu wa kupambana na haki za wanawake IREP Foundation, walisema zipo dhuluma nyingi ambazo wanawake wanapitia katika Jamii ya Pokot huku wanaodhulumiwa wakikosa ufahamu wa mahali wataripoti visa hivyo.
“Tunawahamasisha wanawake kufahamu kuhusu haki zao katika jamii kwa sababu wengi wao wanapitia dhuluma nyingi katika jamii hasa ya Pokot ila hawafahamu kwamba pia wana haki zao na kwamba wanaweza kuripoti visa hivyo.” Alisema Salome.
Salome aidha alizitaka jamii za kimataifa kutambua umuhimu wa mwanamke katika jamii huku akiwasuta wanaume wanaowakandamiza wake zao.
“Nawaambia jamii ya dunia kwamba bila mwanamke hii dunia haitasonga mbele. Hivyo tukichunga wanawake wetu ni kama tumechunga dunia kwa sababu hao ndio wanaohakikisha kwamba sote tuko sawa.” Alisema.
Mbali na Wakfu wa IREP, viongozi wa Mpango wa AJIRA wakiongozwa na Stephen Siwa walikuwapo katika hafla hiyo, lengo lao likiwa kuwahamasisha wanawake kutumia mtandao katika kuripoti dhuluma zozote wanazozipitia mbali na kutumia mtandao pia kujinufaisha kibiashara.
“Kwa muda mrefu wanawake wametengwa katika maswala ya teknolojia. Ila sasa tunasisitiza kwamba wanawake pia wana nafasi sawa na wanaume katika maswala ya mitandao, na tunataka watumie mitandao hiyo ili waweze kujinufaisha.” Alisema Siwa.