MASHIRIKA MBALI MBALI YAPIGA JEKI JUHUDI ZA KUIMARISHA ELIMU YA MTOTO WA KIKE POKOT MAGHARIBI.


Zaidi ya wanafunzi 300 kutoka shule mbali mbali kaunti hii ya Pokot magharibi wamenufaika na vitambaa vya hedhi kwa wanafunzi wa kike pamoja na mavazi ya ndani kwa wanafunzi wa kiume katika shughuli ambayo ilitekelezwa katika shule ya upili ya wasichana ya Nasokol.
Kulingana na mwanzilishi na mkurugenzi wa shirika la Pendo afrika Faith Tanui hatua hiyo ililenga kuhakikisha kuwa mwanafunzi wa kike anaendelea na masomo yake bila kutatizika na pia kuwazuia dhidi ya kulazimika kujihusisha na maswala ya kimapenzi ili kupata vitambaa hivyo, kauli iliyosisitizwa na mhasisi wa shirika la Padmad ambaye ni mshirika katika kampeni hiyo.
Kwa upande wake bingwa wa mbio za marathon Eliud Kipchoge aliyekuwepo katika hafla hiyo ambayo pia ilihusu kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi hao ametoa wito kwa wanafunzi wa kike waliopata ujauzito na kisha kujifungua kurejelea masomo kwani kujifungua sio mwisho wa maisha.
Wanafunzi walionufaika na msaada huo wameelezea furaha yao wakisema hatua hiyo itawawezesha kupata wakati mzuri wa kuhudhuria masomo yao bila wasiwasi ambao mara nyingi hutokea wakati wanapopata hedhi.