MASHAMBULIZI YA WEZI WA MIFUGO YASALIA MWIBA BONDE LA KERIO LICHA YA OPARESHENI YA POLISI.

Mbunge wa Baringo kusini Charles Kamuren anaitaka serikali kuimarisha mikakati yake ya kukabiliana na washukiwa wa wizi wa mifugo wanaoendeleza uvamizi kila mara kwenye kaunti za bonde la kerio.

Kulingana na Kamuren, mikakati iliyotangazwa na waziri wa usalama wa ndani Prof. Kithure Kindiki ikiwamo amri ya kutokuwa nje usiku haijasaidia katika kuwadhibiti majangili.

Kamuren aidha alielezea kusikitishwa na ongezeko la visa vya uvamizi vinavyoripotiwa tangu serikali ilipotangaza opareheni ya kuwakabili wahalifu kwenye kaunti hizi.

“Hii ni hali mbaya zaidi ambayo nimewahi kushuhudia. Na sijui ni nani ambaye anahujumu shughuli hii ya kuwaondoa wahalifu eneo hili. Uvamizi wa hawa majangili umezidi hata kuliko jinsi ilikuwa awali. Na ndio nauliza serikali hii curfew ambayo mlileta huku ni ya nini?” Alisema Kamuren.

Kauli yake ilijiri wakati ambapo wakazi wa eneo la Nosukoru wameelezea kuishi kwa hofu kufuatia uvamizi wa ijumaa wiki iliyopita ambapo afisa wa polisi wa akiba NPR alipigwa risasi na kujeruhiwa mguuni.

“Hawa majangili sasa wanataka kila siku mtu akitoka hospitali mwingine anarudishwa huko? Sasa eneo hili limekuwa hatari hata kuliko awali. Ni juzi tu wamevamia kijiji hiki na kutoweka na mifugo huku afisa wa NPR akipigwa risasi mguuni.” Walisema wakazi.