MAONYESHO YA KILIMO POKOT MAGHARIBI YAANZA RASMI WAKULIMA WAKITAKIWA KUKUMBATIA TEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA KILIMO.

Wakulima katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kukumbatia teknolijia ya kisasa katika kuendeleza shughuli zao za kilimo ili kuwa katika nafasi bora ya kuimarisha mazao yao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa maonyesho ya kilimo ambayo yanaandaliwa katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Kishaunet, naibu gavana kaunti kaunti hiyo Robert Komole alisema kwamba ni kupitia kukumbatia teknolojia ya kisasa ambapo kilimo kitaimarika na kuinua uchumi wa kaunti hiyo.

“Kama serikali ya kaunti tumesema kwamba ni lazima tuinue uchumi wetu kwa kutumia teknolojia tulizo nazo katika kuendeleza kilimo. Tunawataka wakulima wakumbatie teknolojia hizi za kisasa ambazo zitawasaidia pakubwa kuimarisha mazao yao.” Alisema Komole.

Kauli yake ilisisitizwa na waziri wa kilimo na mifugo kaunti hiyo Wilfred Longronyang ambaye aidha alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima kutilia maanani mawaidha ambayo yanatolewa na maafisa wa kilimo ambao wamepewa mafunzo kuhusu jinsi ya kuendeleza kilimo.

“Tunawaomba wakulima kutumia maonyesho haya ya kilimo kupata ushauri wa jinsi ya kuimarisha kilimo kwani pia kutakuwa na maafisa waliopata mafunzo kuhusiana na jinsi ya kuendeleza kilimo ambacho kitawapa wakulima mapato kufuatia juhudi zao.” Alisema Longronyang.

Afisa mkuu katika wizara hiyo Nomi Lemre alisema kwamba maonyesho hayo yatatumika pia kubadili dhana kwamba kaunti ya Pokot magharibi si salama, ikizingatiwa watu kutoka maeneo mbali mbali nchini wanahudhuria maonyesho hayo kauli ambayo ilisisitizwa na waziri wa utumishi wa umma kaunti hiyo Martine Lotee.

“Kwa miaka mingi kaunti yetu imekuwa na sifa mbaya ya utovu wa usalama. Tunalenga kutumia maonyesho haya kudhihirishia ulimwengu kwamba kaunti hii ni salama na si jinsi ambavyo imekuwa ikidhaniwa.” Alisema Lemre.

Wakulima na wafanyibiashara mbali mbali ambao wanahudhuria maonyesho hayo wamepongeza uongozi wa kaunti kwa kuhakikisha kwamba yanarejeshwa hasa baada ya kutokuwepo kwa miaka mingi wakisema yatawafaa zaidi hasa katika kupata ujuzi wa kuendeleza shughuli zao za kilimo.

“Tunafurahia sana maeonyesho haya kwa sababu kwa miaka mingi hatujakuwa na majukwaa ya kuonyesha bidhaa tulizo nazo. Lakini kwa leo tunashukuru kaunti yetu kwa kuandaa maonyesho haya ambapo pia tutapata kujifunza kutoka kwa wakulima kutoka maeneo mengine ya nchi.” Walisema.