Manispaa ya Kapenguria yaendeleza vikao na wakazi kuhusu sheria za mji

Na Benson Aswani,
Uongozi wa manispaa ya Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi unaendeleza vikao na wakazi wa manispaa hiyo katika mikakati ya kutunga sheria ambazo zitasaidia katika kupangilia mji wa makutano.


Naibu meneja wa manispaa hiyo Lydia Tabut alisema kwamba kando na kuweka sheria, vikao hivyo vinalenga kuwahamasisha wakazi hasa wafanyibishara mjini Makutano kuhusiana na maswala ambayo wanapasa kuzingatia wanapoendeleza shughuli zao.

Tabut alisema lengo kuu la mchakato huu mzima ni kuhakikisha mji wa makutano unaafikia viwango ambavyo vinahitajika kupata kibali cha kutangazwa jiji kuu kando na kuwavutia wahisani ambao watasaidia katika maendeleo.


“Hizi sheria ambazo tunawaeleza watu wetu zitatasaidia mji wetu kuendelea vizuri na kupata hadhi ya kutangazwa kuwa jiji. Kupitia sheria hizi pia manispaa yetu itapata wahisani wa kutuletea ufadhili,” alisema Bi. Tabut.


Hata hivyo Tabut alielezea kuridhishwa na hatua ambazo zimepigwa kufikia sasa katika mipangilio ya mji wa Makutano ikilinganishwa na miaka ya awali, hatua ambazo alisema zimetokana na ushirikiano wa serikali ya kaunti.


“Manispaa ya Kapenguria imekuwa nzuri kuliko ilivyokuwa hapo nyuma ambapo hakukuwa na mipangilio mizuri. Tunashukuru serikali ya gavana Kachapin kwa kuwa imetuunga mkono kikamilifu na kutuwezesha kufika mahali tupo sasa hivi,” alisema.