MAMLAKA YA MAJANGA YAIKABIDHI SHULE YA UPILI YA KIWAWA MAGODORO 30 BAADA YA BWENI LA SHULE HIYO KUTEKETEA.
Na Benson Aswani.
Maafisa kutoka idara inayoshughulikia majanga katika kaunti ya Pokot magharibi wamezuru shule ya upili ya wavulana ya Kiwawa eneo la Kacheliba kutathmini uharibifu uliosababishwa na moto ambao ulizuka shuleni humo jumatatu alfajiri.
Maafisa hao wakiongozwa na Koslol Pius waliikabidhi shule hiyo msaada wa magodoro 30 na vifurushi viwili vya blanketi wakiahidi kutoa mafunzo ya kukabiliana na moto kwa walimu wa shule hiyo ili kuwa katika nafasi bora ya kukabili mikasa kama hiyo iwapo itatokea tena siku za usoni.
“Tumefika hapa na kushuhudia kwamba bweni moja la watoto zaidi ya 140 lilishika moto na kuteketea. Hivyo kama kaunti tumeweza kuleta bidhaa kidogo hapa za kuwasaidia wanafunzi walioathirika. Pia tutawapa mafunzo baadhi ya walimu ili kuasaidia kukabili mikasa kama hii inaposhuhudiwa.” Walisema.
Uongozi wa shule hiyo ukiongozwa na mwalimu mkuu Luke Lotukoi ulikadiria kuwa kila mwanafunzi alipoteza bidhaa za thamani ya shilingi takriban alfu 44, ukipongeza mamlaka hiyo kwa msaada huo na kutoa wito kwa wahisani zaidi kujitokeza ili kuwafaa wanafunzi walioathirika.
“Mwanafunzi mmoja alipoteza bidhaa za thamani ya shilingi alfu 44,390 kwenye mkasa huo na tunashukuru serikali kwa msaada huu ambao tumepewa. Tunaomba wahisani zaidi kujitokeza ili watusaidie kuhakikisha kwamba wanafunzi hao wanapata bidhaa zinazohitajika.” Alisema Lotukoi.
Ni wito ambao ulikaririwa na chifu wa eneo hilo Jackson Kesamur ambaye alisema kwamba huenda wanafunzi waliopoteza bidhaa zao kwenye mkasa huo wakakumbana na changamoto katika kuendeleza shughuli za masomo iwapo hawatapata msaada.
“Huenda wengi wa wanafunzi ambao walipoteza bidhaa zao kwenye mkasa huo wa moto wakapitia changamoto katika kuendeleza elimu yao iwapo hawatasaidiwa. Hivyo tunaomba wale ambao wanaweza kutupa usaidizi kufanya hivyo.” Alisema Kasemur.