MALUMBANO YAENDELEA KATI YA NATEMBEYA NA CHRIS WAMALWA KUHUSU UONGOZI WA TRANS NZOIA.


Mshirikishi wa serikali eneo la Bonde la ufa George Natembeya amepuuza juhudi za mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha kiti cha ugavana wa kaunti ya Trans nzoia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutaka kuungwa mkono kutoka kwa wakazi wa kaunti hiyo.
Natembeya amesema kuwa mbunge wa eneo bunge la Kiminini Chris Wamalwa hana tajriba ya kutosha kuwania kiti cha ugavana.
Natembeya ambaye anawania kiti hicho kupitia chama cha DAP-K amejipigia debe kuwa chaguo bora kwa misingi kuwa ana uzoefu mkubwa wa miaka 25 katika utenda kazi serikalini huku Wamalwa ambaye anawania kiti hicho kupitia chama cha Ford Kenya akiwa na uzoefu wa miaka 10 pekee katika siasa.
Kutokana na hilo Natembeya sasa anamshauri Wamalwa kuwania kiti cha uwakilishi wadi au uspika.
Kauli ya Natembeya inajiri wakati wandani wa Ruto wakiongozwa na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen waliokuwa wakizungumza katika kaunti hiyo ya Trans nzoia wakiendeleza shutuma dhidi ya Natembeya na kumtaja kuwa asiyefaa kupewa nafasi ya kuwa gavana.