MAKUNDI MAWILI YA KANISA LA ACK ST. ANDREWS MAKUTANO YAENDELEA KUNYOSHEANA KIDOLE KUFUATIA VURUGU ZA JUMAPILI.

Uongozi wa kanisa la St. Andrews ACK mjini Makutano kaunti ya Pokot magharibi umejitetea kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa katika kanisa hilo kwenye ibaada ya jumapili iliyopita.

Mzee wa kanisa hilo Geofrey Lotam ambaye alihusika moja kwa moja kwenye vurugu hizo kwa kuwacharaza baadhi ya waumini viboko alisema kwamba hali hiyo ilianza wakati kundi moja linalong’ang’ania uongozi wa kanisa hilo lilianza kuhitilafiana na ibaada.

Alisema juhudi za mchungaji wa kanisa hilo pamoja na baadhi ya wazee kujaribu kulisihi kundi hilo kukoma kuhitilafiana na ibaada kwa kuanzisha ibaada nyingine kwa ukumbi uo huo ziliambulia patupu hali iliyomlazimu yeye kuchukua hatua hiyo ya kuwacharaza viboko.

“Ibaada ilipoanza kundi hili likaanza ibaada yao kwenye ukumbi uu huu kwa lengo la kuhakikisha kwamba sisi hatuendelei na ibaada yetu. Mchungaji alijaribu kuzungumza nao lakini hawakusikia. Mimi pia nikawaambia waende kufanya ibaada yao sehemu nyingine kama hawataki kushiriki nasi lakini pia wakakataa. Mimi nikalazimika kuchukua hatua ya kuwacharaza nilipoona hali imezidi.” Alisema Lotam.

Lotam alisema kumekuwa na mzozo baina ya makundi mawili katika kanisa hilo tangu mwaka jana ambapo kundi moja limekuwa liking’ang’ani uongozi, viongozi wake wakiridhi mmoja kutoka kwa mwingine kila mara bila ya kufuata katiba ya kanisa hilo.

“ Kumekuwa na mzozo wa uongozi katika kanisa hili tangu mwaka jana, ambapo kuna askofu aliyekuwa hapa, alipostaafu alimkabidhi uongozi askofu mwingine. Huyo pia alipostaafu akataka kulazimishia uongozi kijana yake. Kwa hivyo kama wazee tukaona kanisa hili lina katiba inayoweka wazi jinsi mambo yanapasa kuendeshwa. Kwa hivyo tulipochukua hatua makundi haya yakaibuka na kuanza pingamizi.” Alisema.

Mmoja wa waumini ambao walicharazwa viboko na mzee huyo wa kanisa alishutumu kisa hicho akisema kwamba si mara ya kwanza kwa Lotam kumkabili kwani hali kama hiyo ilitokea awali akiwa mwathiriwa.

“Mimi nilikuwa naimba na nikashutukia tu mtu ananicharaza viboko. Mwaka jana pia kulikuwa na hali kama hii ambapo huyu mzee pia aliniandama mimi. Sasa nashindwa ni shida gani ambayo mimi niko nayo na mzee huyu.” Alisema.