Makamanda wa rais Pokot Magharibi waendelea kutetea utendakazi wake

Na Benson Aswani,
Viongozi mbali mbali wandani wa rais William Ruto katika kaunti ya Pokot Magharibi wameendelea kutetea utendakazi wa serikali ya Kenya kwanza chini ya uongozi wa rais Ruto licha ya ukosoaji mkubwa kutoka mrengo wa upinzani.


Wakiongozwa na katibu katika wizara ya ujenzi Joel Arumonyang, viongozi hao walisifia hatua ambazo zimepigwa chini ya utawala wa rais Ruto ikiwemo kuimarika sekta ya kilimo pamoja na miradi ya kuwainua vijana kiuchumi ambayo inaendelezwa na serikali ya Kenya kwanza kote nchini.

“Serikali yetu imejaribu sana katika kuimarisha maisha ya wananchi. Tunaona sasa kuna uzalishaji mzuri wa chakula kutokana na mbolea ya bei nafuu pamoja na kutoa fedha kwa makundi ya vijana na kina mama kuimarisha hali yao ya uchumi,” alisema Arumonyang.


Kauli yake imesisitizwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye alidai kuwepo viongozi wenye nia ya kuhujumu juhudi za rais William Ruto kuimarisha maisha ya wananchi, akiwataka kumpa muda wa kutekeleza yale ambayo aliwaahidi wananchi wakati wa kampeni.


“Kuna wale ambao wana dhana kwamba Kenya ni yao. Na ndio maana watu wengine wakiwa katika uongozi wanasema kwamba hawafai. Hii Kenya ni yetu sote na rais wetu anafaa kupewa muda wa kuwahudumia wananchi alivyowaahidi,” alisema Lochakapong.


Kwa upande wake mwakilishi kina mama Rael Kasiwai alitoa wito kwa wakazi wa kauti ya Pokot magharibi kuunga mkono serikali ya rais Ruto kutokana na yale ambayo imeweza kuafikia ikiwemo kuajiri idadi kubwa zaidi ya walimu na kuboresha sekta ya kilimo miongoni mwa maswala mengine.


“Rais wetu amefanya kazi nzuri ikiwemo kuwaajiri zaidi ya walimu 76,000 ambayo haikuwahi kutokea. Kwa hivyo nawaomba watu wetu kuendelea kumuunga mkono ili aendelee kuimarisha Kenya,” alisema Kasiwai.