Mahakama ya Kapenguria yazindua kitengo cha upatanishi

Hakimu Wa Mahama Ya Kapenguria Stelah Telewa {kulia} Akifungua Afisi ya Kitengo cha Upatanishi ,Picha/Benson Aswan

Na Benson Aswani,
Mahakama kuu ya Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi imezindua rasmi kitengo cha upatanishi ‘Court Annexed Mediation’ katika mahakama hiyo kitakachosaidia katika kusuluhisha kesi mbali mbali kama njia moja ya kupunguza mirundiko ya kesi mahakamani.


Akizungumza kwa niaba ya hakimu mkuu wa mahakama hiyo Stelah Telewa wakati wa uzinduzi wa kitengo hicho, naibu msajili wa mahakama hiyo Chelagat Kenei alisema kitengo hicho kinatambuliwa kisheria na kinaongozwa na maafisa walioidhinishwa na mahakama.


“Katiba ya Kenya inatambua utumizi wa mbinu mbadala za kusuluhisha kesi, na kitengo cha upatanishi ni moja ya njia mbadala za kusuluhisha kesi pamoja na kuhakikisha kwamba uhusiano mwema baina ya pande mbili unadumishwa,” alisema Bi. Kenei.


Kulingana na jaji wa mahakama hiyo Linus kasan, maafisa wanaojukumiwa wajibu huo wamepokea mafunzo maalum ya jinsi ya kushughulikia kesi hizo, wakati uo huo wakihakikisha wanaimarisha uhusiano baina ya pande zinazozozana akisisitiza huduma hiyo haigharimu wahusika fedha zozote.


“Kitengo hiki kinaendeshwa na watu ambao wamepokea mafunzo ya jinsi ya kusuluhisha kesi hizi na kuhakikisha kwamba wanaozozana wanadumisha uhusiano wao mwema,” alisema jaji Kasan.


Ni hatua ambayo ilipongezwa na wakili wa mahakama ya Kapenguria Geofrey Lowasko ambaye alisema kando na kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani, itasaidia kuimarisha uhusiano miongoni mwa wakazi hasa wanaozozana.


“Kitengo hiki kitasaidia pakubwa kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani pamoja na kudumisha amani katika jamii,” alisema Bw. Lowasko.