MAHAKAMA YA JUU YAANZA VIKAO VYA KUSIKILIZA KESI YA KUPINGA USHINDI WA RUTO.


Jopo la majaji 7 wa mahakama ya juu hatimaye limeanza vikao vyake vya kusikiliza rufaa kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais likiwa limeweka maswala 9 makuu kwenye rufaa hizo ambayo yatatumika katika kuafikia uamuzi.
Jopo hilo ambalo linaongozwa na jaji mkuu Martha Koome na naibu wake Philomena Mwilu limesema maswala hayo ni yakiwemo iwapo teknolojia iliyotumiwa na tume ya uchaguzi IEBC kwenye uchaguzi wa agosti 9 ilikuwa ya kuthibitishwa.
Aidha jopo hilo litabaini iwapo kulikuwepo na udukuzi wa mtandao wa IEBC wakati wa kutundika fomu za 34a.
Katika taarifa jaji mkuu Martha Koome ameongeza kwamba majaji watabaini iwapo kuna tofauti zozote za matokeo ya uchaguzi kwenye fomu za 34a zilizowekwa mtandaoni ikilinganishwa na zile zilizowasilishwa mbele ya tume hiyo.
Aidha mahakama imeafikia kwamba pande zinaohusika kwenye rufaa hiyo zinafaa kufahamu iwapo kuahirishwa kwa uchaguzi kwenye maeneo manane kuliathiri idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki uchaguzi.
Maswala ambayo mahakama italenga kubaini na kuwa msingi wa uamuzi wake ni iwapo IEBC ilithibitisha, kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais kuambatana na kipengele cha 138 katika sehemu ya tatu hadi sehemu ya kumi.
Aidha majaji watabaini iwapo rais mteule William Ruto alipata asilimia 50 ya kura na kura moja zaidi jinsi inavyohitajika kikatiba.