MAENEO YA MIPAKANI YATAJWA KUWA CHANGAMOTO KATIKA VITA DHIDI YA UKEKETAJI POKOT MAGHARIBI.


Shirika la world Vision limeelezea kuafikia ufanisi mkubwa katika vita dhidi ya dhuluma za kijinsia ikiwemo ukeketaji na kuozwa mapema watoto wa kike eneo la Alale katika kaunti ya Pokot magharibi kupitia mafunzo ambayo limetoa kwa wenyeji wa eneo hilo.
Kulingana na afisa wa shirika hilo Teresa Cheptoo wamelenga zaidi eneo hilo la mpakani kutokana na hali kuwa wanaotekeleza uovu huo wamekuwa wakitorokea taifa jirani la Uganda hali aliyosema kwamba imekuwa changamoto kumaliza dhuluma hizo.
“Tumelenga zaidi eneo hili la Alale katika mafunzo yetu kwa wakazi kuhusiana na dhuluma za kijinsia na tunaona kwa kiwango fulani tumepata ufanisi. Tumekuwa na changamoto kubwa kukabili visa hivi kwa sababu wengi wa wanaotekeleza wanavuka taifa jirani la Uganda.” Alisemas Cheptoo.
Ni kauli iliyosisitizwa na naibu chifu wa eneo hilo Celina Liman ambaye aidha alisema kwamba wanakabiliwa na uchache wa vituo vya kuwahifadhi watoto wa kike ambao wanakabiliwa na tishio la kukeketwa au kuozwa mapema.
“Sheria zetu zinatuzuia kuwafuata wanaoendeleza ukeketaji wa watoto wa kike ambao wanavuka hadi taifa jirani la Uganda na hii imekuwa changamoto kuu katika vita hivi. Na pia tunakumbwa na changamoto ya sehemu ya kuwahifadhi waathiriwa kwani kwa sasa tuna kituo kimoja pekee.” Alisema Liman.
Aidha Cheptoo alisema kwamba wanahusisha vijana wa kiume katika mafunzo hayo ili kuwawezesha kufahamu machungu wanayopitia watoto wa kike wanapokeketwa na kupata mchango wao katika juhudi za kuimarisha vita dhidi ya tamaduni hiyo dhalimu.
“Kwa muda mrefu swala la ukeketaji limekuwa tu kuhusu watoto wa kike ila tulitambua kwamba tumefanya machache sana kuhusiana na swala hilo. Na hivyo tukaamua kwamba tutawahusisha watoto wa kiume katika vita hivi ili waelewe wanayopitia watoto wa kike wanaokeketwa, na tumeona hatua hii imezaa matunda.” Alisema Cheptoo.