MADHARA YA MVUA YAANZA KUSHUHUDIWA, WAFANYIBIASHARA WAKIKADIRIA HASARA ORTUM.
Wafanyibiashara katika soko la Ortum kaunti ya Pokot mgharibi wanakadiria hasara kufuatia maporomoko ya ardhi ambayo yalikumba soko hilo na kuharibu mijengo pamoja na barabara kutokana na mvua kubwa ambayo inaendelea kushuhudiwa nchini.
Akizungumza jumapili alipozuru soko hilo kutathmini hali ilivyo, gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin aidha alisema kwamba mtu mmoja hajulikani aliko, ikikisiwa huenda alisombwa na maji kufuatia mafuriko makubwa yaliyoshuhudiwa eneo hilo huku pikipiki yake ikipatikana.
“Sehemu kubwa sana ya soko la Ortum imeporomoka. Kumeshuhudiwa hasara kubwa kwa wafanyibiashara wa soko hili kwa sababu majengo yao yamebomolewa. Lakini baya zaidi ni kwamba kuna mtu ambaye hajulikani aliko. Inakisiwa huenda alisombwa na maji kwa sababu pikipiki aliyokuwa akitumia ilipatikana.” Alisema Kachapin.
Kachapin aliwataka wakazi ambao wanaishi karibu na mito kuhama maeneo hayo na kutafuta sehemu salama huku akisisitiza haja ya wakazi kuhifadhi mazingira na kutolima sehemu za miinuko, hatua aliyosema kwamba ndiyo suluhu ya kudumu kwa swala la mafuriko na maporomoko ya ardhi.
“Wale wanaoishi karibu na mito wakati huu ambapo kunaendelea kushuhudiwa mvua tunawapa tahadhari kwamba waweze kuhamia maeneo salama. Ila suluhu ya kudumu kwa hali hii ni kuhifadhi mazingira na wakazi kuacha kulima maeneo ya miinuko.” Alisema.
Kwa upande wake naibu gavana wa kaunti hiyo Robert Komole aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo walioathirika na mafuriko hasa wafanyibiashara ambao ndio waathiriwa wakuu kwamba serikali ya kaunti itasimama nao.
“Tunasikia kwamba watu hawakulala huku Ortum. Tumezunguka soko lote la Ortum na tumeyaona madhara ambayo yamesababishwa. Kwa hivyo nawahakikishia kwamba serikali ya kaunti iko pamoja nanyi kwa hili.” Alisema Komole.