MACHIFU WALAUMIWA KWA KUTUMIA NGUVU KUPITA KIASI KUKABILI UGEMAJI WA POMBE HARAMU POKOT MAGHARIBI.

Familia moja eneo la Kambi chafu katika kaunti ya Pokot magharibi inalilia haki kufuatia kisa cha kujeruhiwa mama yao baada ya kudaiwa kuvamiwa na chifu wa eneo hilo.

Wakiongozwa na Amila lodio jamaa hao walisema chifu huyo pamoja na wenzake walifika katika boma lao kwa madai ya kuendeleza msako dhidi ya ugemaji wa pombe haramu, na kuanza kuharibu vifaa vyao kabla ya kumvamia mama yao na kumjeruhi vibaya kwa madai ya kujaribu kuzuia oparesheni hiyo.

“Machifu walikuwa wakifanya msako wa biashara ya ugemaji wa pombe haramu. Sasa walianza kupasua vyombo hapa na mama alipoenda kuchukua beseni ambayo ilikuwa ikipasuliwa, chifu akamgonga kwa chuma kichwani. Alikuwa na chuma hiyo mkononi niliiona kwa macho yangu.” Alisema Lodio.

Ni kisa ambacho kimesutwa vikali na mwakilishi wadi maalum Bruno Lomeno ambaye alimtaka kamishina wa kaunti hiyo Apolo Okelo kumchukulia hatua chifu huyo na naibu kamishina wa Kongelai kwa kutumia oparesheni hiyo kuendeleza dhuluma dhidi ya wakazi.

“Huo msako ni wa kisheria hatukatai. Lakini tabia ya machifu kuwapiga raia kwa kisingizio cha kuendesha oparesheni dhidi ya pombe haramu hatutakubali. Kwa hivyo, namtaka kamishina wa kaunti hii ahakikishe kwamba naibu kamishina eneo hilo na huyo chifu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.” Alisema Bruno.

Hata hivyo naibu chifu wa Kongelai Luke Lorita alikana madai hayo akisema huenda mama huyo alijeruhiwa kwingine na kutumia kisingizio hicho kuhitilafiana na oparesheni dhidi ya ugemaji wa pombe ambayo inaendelezwa na maafisa wa usalama.

Sina ufahamu wowote wa raia kupigwa na chifu. Huyu labda ni mtu ambaye alikuwa akitoroka oparesheni hiyo na akakutana na mambo yake huko, sasa anatumia kisingizo hicho kurudisha nyuma hii shughuli.” Alisema Lorita.