MACHIFU WALAUMIWA KWA KUKITHIRI UTOVU WA USALAMA KERIO VALLEY.


Mshirikishi wa usalama eneo la bonde la ufa maalim Mohammed amewalaumu maafisa wa usalama maeneo ya mashinani katika kaunti zinazopatikana bonde la kerio kufuatia kukithiri utovu wa usalama ambao unasababishwa na wezi wa mifugo.
Akizungumza baada ya kukutana na machifu pamoja na vitengo mbali mbali vya usalama kaunti hii ya Pokot magharibi, Maalim amewalaumu maafisa hao kwa kutokuwa na umakinifu wa kufahamu mipango ya wahalifu na kutoa mapema habari kwa maafisa wa polisi ili hatua kuchukuliwa.
Aidha Maalim amewakosoa baadhi ya machifu kwa kuendesha shughuli zao maeneo ya mijini hali inayowapelekea kutofahamu kinachoendelea maeneo ya mashinani, akisema kuwa wanatakiwa kisheria kuwa karibu na mawananchi mashinani.
Wakati uo huo Maalim amewaonya maafisa hao dhidi ya kujihusisha na maswala ya ubugiaji pombe kwani ni jukumu lao kuhakikisha kuwa ugemaji wa pombe haramu unakabiliwa maeneo yao ikizingatiwa ni waakilishi wa serikali maeneo hayo.