MACHIFU TRANS NZOIA WAANZISHA OPARESHENI YA KUWASAKA VIJANA AMBAO HAWAJACHUKUA VITAMBULISHO.
Na Benson Aswani
Ikiwa zimesalia siku 9 kabla ya kutamatika zoezi la kuwasajili wapiga kura machifu na manaibu wao katika kaunti ya Trans nzoia wameendeleza harakati za kuwasaka wale ambao hawajachukua vitambulisho vyao vilivyoko katika afisi za serikali na kuwapeleka katika vituo vya kujisajili kuwa wapiga kura.
Wakiongozwa na Charles Namunyu, machifu hao wamesema kuwa wanashirikiana na idara ya usajili wa watu kaunti hiyo kuafikia hilo kutokana na hali kuwa kaunti hiyo ya Trans nzoia imesajili idadi ya chini mno ya wapiga kura kufikia sasa kinyume na idadi iliyokuwa ikikadiriwa na tume ya IEBC.
Namunyu ametumia fursa hiyo kuwasihi vijana katika kaunti hiyo ambao hawajasajiliwa kutumia kipindi kilichosalia kuhakikisha kuwa wanasajiliwa kwani ndiyo njia ya pekee ya kuhakikisha wanatekeleza jukumu lao la kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaowapendelea katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.