Mabadiliko ya tabia nchi yapelekea vipindi visivyotabirika vya mvua

Wilson Lonyang’ole Mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya anga kaunti ya pokot magharibi, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Maeneo mengi ya kaunti ya Pokot magharibi hasa nyanda za chini ikiwemo pokot ya kaskazini yatapokea mvua chache katika kipindi hiki cha mwezi aprili.
Katika kikao na wadau wakati akitoa ripoti ya idara ya hali ya anga ya mwezi Aprili, mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya anga kaunti hiyo Wilson Lonyang’ole aliwahimiza wakazi wa maeneo hayo kupanda mimea ambayo itastahimili mvua chache.
Aliwashauri wakulima kupata ushauri kutoka kwa maafisa wa kilimo kuhusu mbegu bora ambazo zitanawiri maeneo hayo.
Aidha Lonyang’ole aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kukumbatia zoezi la upanzi wa miti na kuhifadhi mazingira ili kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi, ambayo alisema yamechangia pakubwa vipindi vinavyobadilika vya mvua.
“Tunatarajia kiwango kidogo sana cha mvua mwezi huu wa Aprili katika nyanda za chini, ambapo wakulima wanapasa kuzingatia zaidi kupanda mimea ambayo itastahimili mvua chache. Nawashauri wakulima maeneo hayo kupata ushauri kutoka kwa wataalam kuhusu aina za mimea ya kupanda,” alisema Lonyang’ole.
Hata hivyo Lonyang’ole alisema nyanda za juu za kaunti hiyo zitaendelea kushuhudia viwango vya juu vya mvua hasa kuanzia juma lijalo akiwahimiza wakulima ambao bado hawajapanda mimea kufanya hivyo.
“Nyanda za juu zitaendelea kushuhudia mvua ya wastani, na hapa wakulima ambao labda hawajapanda wanafaa kutumia kipindi hiki kuendeleza shughuli ya upanzi kwani kuanzia juma lijalo kiwango cha mvua kitaongezeka,” alisema.