MAANDAMANO YA WAKULIMA WA MIWA KULALAMIKIA USIMAMIZI WA KIWANDA CHA NZOIA YASITISHWA


Mbunge wa Kanduyi kaunti ya Bungoma Wafula Wamunyinyi amefanikiwa kutuliza maandamano ya wakulima wa miwa ambayo yaliratibiwa kufanyika leo kushinikiza kuondolewa madarakani mkurugenzi mkuu wa kiwanda cha miwa cha nzoia michael makokha.
Hii ni baada ya mbunge huyo kufanya mkutano na wakulima wafanyikazi wa kiwanda hicho na viongozi wa miungano ya wakulima pamoja na mashirika mbali mbali ya kijamii kutafuta suluhu ya matatizo ambayo yanakumba kiwanda hicho.
Wakulima hao wamesema kuwa wanadai kiwanda hicho takriban shilingi milioni 70 ambazo ni malipo ya miezi saba.
Katika kikao na wanahabari wamunyinyi amesema kuwa wakulima wameafikiana kusitisha maandamano na kumpa makokha muda wa mwezi mmoja kushughulikia matakwa yao.
Aidha wamunyinyi amesema usimamizi wa kiwanda hicho utabuni mfumo wa kuhakikisha kuwa wakulima na wafanyikazi wengine wanapata malipo yao kwa wakati ufaao.
Wakati uo huo Makokha amewahakikisha wakulima kuwa kiwanda hicho kitatekeleza maswala yote ambayo wameafikiana akiwahimiza kushirikiana kwa manufaa ya eneo hilo la magharibi ya nchi.