MAANDAMANO YA MRENGO WA AZIMIO YATAJWA KUWA UCHOCHEZI DHIDI YA SERIKALI YA RAIS RUTO.

Viongozi mbali mbali wanaoegemea mrengo wa Kenya kwanza wameendelea kukosoa maswala ambayo yanashinikizwa na kinara wa chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya Raila Odinga na vinara wenza katika maandamano ambayo wanaendeleza nchini.

Wa hivi punde kukosoa maandamano hayo ni mwakilishi wadi ya Siyoi katika kaunti ya Pokot magharibi Esther Serem ambaye alisema kwamba shinikizo za Raila kutaka kufunguliwa sava miezi saba baada ya kukamilika uchaguzi mkuu wa mwaka jana zina njama fiche.

“Kile ambacho sikubaliani na muungano wa azimio ni shinikizo za kutaka sava zifunguliwe. Sioni ni kwa nini Raila asubiri hadi baada ya miezi saba ndio aanze kuitisha kufunguliwa sava. Hapo mimi naona ni kama kuna malengo fiche.” Alisema Serem.

Aidha Serem alimsuta Raila kwa kile alidai alisalia kimya gharama ya maisha ikiwa juu katika utawala wa rais mustaafu Uhuru Kenyatta na inashangaza kumwona akiandaa maandamano katika utawala wa Ruto ambaye kulingana naye anajitahidi kuboresha hali ya maisha ya mwananchi.

“Wakati wa rais mustaafu Uhuru Kenyatta ,unga ilikuwa zaidi ya shilingi 200 ila hakupiga kelele lakini sasa unga imefika karibu shilingi 180. Mbona sasa anasumbua watu? Kwa hivyo japo tuna haki ya kuandaa maandamano lakini yake naona ni kama ni uchochezi.” Alisema.

Serem sasa anataka viongozi kudumisha utulivu nchini ili kumpa rais William Ruto mazingira bora ya kutekeleza miradi ya maendeleo aliyoahidi wakenya, na kisha kupimwa kazi yake baada ya kipindi cha miaka mitano.

“Tunaomba tu kwamba viongozi wetu wake chini, wazungumze na kumaliza mvutano huu ili tuwe na nchi ya amani na tumpe rais Ruto nafasi ya kuhudumia wakenya. Tutampima rais baada ya miaka mitano iwapo hatakuwa amefanya kazi vizuri basi tutampa mtu mwingine nafasi ya kuongoza.” Alisema.