MAANDAMANO YA AZIMIO YATAJWA KUWA TISHIO KWA OPARESHENI YA KIUSALAMA KASKAZINI MWA BONDE LA UFA.

Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameelezea hofu kwamba huenda maandamano ambayo yanaendelezwa na chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya maeneo mbali mbali ya nchi kushinikiza kupunguzwa gharama ya maisha, yakaathiri oparesheni ya usalama ambayo inaendelezwa katika kaunti za kaskazini mwa bonde la ufa.

Katika mkao na wanahabari Poghisio alisema huenda maafisa wanaoendeleza oparesheni hiyo ya usalama wakaondolewa maeneo haya na kupewa majukumu mengine ya kukabili maandamano ambayo sasa yanaendelezwa kote nchini.

Poghisio alisema hali hii inapelekea taifa kurudi nyuma pakubwa katika hatua ambazo limepiga kuafikia amani na utulivu, akiwalaumu wanasiasa wanaowazingira wahusika wakuu upande wa serikali na upinzani kwa kuwapotosha rais William Ruto na kinara wa upinzani raila Odinga kuhusiana na hali ilivyo nchini.

“Hali inavyoendelea naona sasa maafisa wa polisi wataondolewa huku na kutumwa sehemu nyingine kudhibiti maandamano ambayo sasa yameenea kote nchini.  Hali ilivyo naona tunarudi nyuma sana kwa hatua ambazo tumepiga kuafikia amani na utulivu nchini. Nawalaumu washauri wa hawa watu wawili kwa kuwapa ushauri wa kuwapotosha wa kushikilia misimamo yao.” Alisema Poghisio.

Poghisio sasa anatoa wito kwa rais William Ruto na Raila Odinga kulegeza misimamo yao na kuketi chini ili kuandaa mazungumzo yatakayopelekea kupatikana suluhu ya kudumu kwa hali ambayo inashuhudiwa nchini na kuwaruhusu wananchi kuendelea na shughuli za kulijenga taifa.

“Katika hali kama hii, mwisho wa siku ni mwananchi wa kawaida ambaye ataumia kwa sababu sasa hakuna maendeleo ambayo yataafikiwa kwa taifa ambalo halina amani. Kwa hivyo mimi nawashauri tu viongozi wa pande zote mbili kulegeza misimamo yao na kuandaa mazungumzo ili kupata suluhu.” Alisema.

Ikumbukwe muungano wa azimio ulitangaza maandamano ya siku tatu kuanzia jumatano hadi ijumaa ili kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha.