MAANDALIZI YA MITIHANI YA KITAIFA YAKAMILIKA POKOT MAGHARIBI.


Wito umetolewa kwa wasimamizi wa vituo mbali mbali vya mitihani katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuwa makini na kutoruhusu hali yoyote isiyo ya kawaida ikiwemo udanganyifu kushuhudiwa wakati wa mitihani ya kitaifa ambayo inatarajiwa kuanza mwezi machi mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kikao cha wadau katika sekta ya elimu cha maandalizi ya mitihani hiyo kilichofanyika katika shule ya upili ya Cheokorniswo, naibu kamishina eneo la Kipkomo Teresia Mugure amesema kuwa kwa ushirikiano na wakuu wa elimu kaunti hii wataandaa ziara za kushtukiza katika vituo mbali mbali kuhakikisha kuwa sheria zote zinazingatiwa katika usimamizi wa mitihani.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na mkurugenzi wa elimu eneo la Kipkomo Evans Onyancha ambaye aidha amesema kuwa wameweka mikakati ya kuzia hilo kando na kuhakikisha yapo magari yatakayotumika katika usafirishaji mitihani hadi maeneo ambako kuna tatizo la usafiri.
Wakuu wa shule mbali mbali waliohudhuria kikao hicho wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Chepkorniswo John Cheruo wameelezea matumani ya mitihani hiyo kufanyika katika mazingira bora kutokana na maadalizi ambayo wamefanya.