MAAFISA WA USALAMA WASHUTUMIWA KWA KUWADHULUMU WAKAZI WAKATI WA KUENDESHA MSAKO LOMUT.

Mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ameshutumu vikali kile ambacho amedai hatua ya maafisa wa jeshi kuendesha msako katika nyumba za wakazi wa eneo la Lomut kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Akizungumza baada ya kuzuru eneo hilo siku moja tu baada ya msako huo, Lochakapong alisema kwamba zaidi ya nyumba 50 zilizokuwa zimefungwa wakati wa msako huo zilivunjwa na maafisa hao aliodai waliharibu mali ya wakazi na hata kuwajeruhi wengine.

Lochakapong aliwasuta maafisa hao kwa kutegemea taarifa potovu za kijasusi kuhusu kuwepo silaha haramu eneo hilo kwani licha ya msako huo uliopelekea hasara kwa wakazi hamna bunduki hata moja iliyopatikana.

“Hiyo jana wanajeshi walikuja hapa mapema sana kuendesha oparesheni kwa nyumba za watu kwa kisingizio cha kutafuta silaha haramu. Nyumba ambazo zilipatikana zimefungwa takriban 57 zilivunjwa, mali ya wananchi ikaharibiwa. Nalaani sana kitendo hiki kwani maafisa ambao wanapasa kuhakikisha usalama wa raia ndio sasa wanakuwa tishio kwa usalama wao.” Alisema Lochakapong.

Kisa hicho pia kilisutwa vikali na mwakilishi wadi ya Lomut David Tong’ole ambaye alisema kimepelekea baadhi ya wakazi kuyahama makazi yao kwa kuhofia usalama, akiitaka serikali kuwafidia wakazi walioathirika na tukio hilo.

“Kitendo hiki kimepelekea wakazi kuanza kuondoka kwa kuhofia usalama wao. Kwa hivyo naomba serikali kuwafidia wakazi ambao waliathiriwa na msako huo. Wakazi ambao nyumba zao zilivunjwa, wakazi ambao vyakula viliibwa na hata pesa kuporwa wapewe fidia.” Alisema Tong’ole.

[wp_radio_player]