MAAFISA WA NPR WATAKIWA KUKAZA KAMBA KATIKA VITA DHIDI YA UHALIFU MIPAKANI PA POKOT MAGHARIBI.

Maafisa wa NPR Pokot Magharibi

Na Benson Aswani.

Afisa wa mipango maalum katika afisi ya gavana kaunti ya Pokot magharibi David Chepelion ametoa wito kwa maafisa wa akiba NPR wanaohudumu maeneo yanayokabiliwa na utovu wa usalama mipakani pa kaunti hiyo kusimama imara na kukabili wahalifu maeneo hayo.

Akizungumza baada ya kuhudhuria mazishi ya afisa wa NPR aliyeuliwa na wahalifu eneo la Lonyang’alem wadi ya Kasei, Chepelion aliwahakikishia maafisa hao kwamba serikali ya gavana Simon Kachapin iko tayari kushirikiana kikamilifu nao kuhakikisha kwamba visa hivyo vinakabiliwa.

Aidha Chepelion alisema kwamba serikali ya gavana Kachapin imeweka mikakati ya kuhakikisha chakula kinawafikia maafisa hao katika oparesheni hiyo pamoja na gari ambalo watakuwa wakilitumia kuendesha doria.

“Tunawaomba maafisa wa NPR kukaa ngumu na kuwahakikishia wakazi wetu usalama kwa ushirikiano na maafisa wa polisi. Gavana wetu Simon Kachapin amehakikisha kwamba maafisa hawa watapewa chakula pamoja na gari ambalo litasaidia kupiga doria.” Alisema Chepelion.

Mwakilishi wadi wa eneo la Kasei Francis Krop alilaani vikali mauaji ya afisa huyo akitaja mizozo kuhusu ardhi kuwa chanzo kikuu cha utovu wa usalama, huku akitoa wito kwa serikali kupitia wizara ya ardhi kubaini mpaka wa kaunti hizi mbili ili kutia kikomo mauaji ya wananchi wasio na hatia.

Ugomvi wetu jamii ya Pokot na Turkana si tena kwa mifugo, ila sasa unahusu swala la ardhi. Tunaomba serikali kupitia idara husika kufika maeneo haya ili kuwasaidia wakazi wa jamii hizi kubaini mipaka ya kaunti hizi mbili, ili tupate suluhu ya kudumu kwa tatizo la utovu wa usalama.” Alisema Krop.