MAAFISA WA KWS WALAUMIWA KWA KUTELEKEZA MAJUKUMU YAO HUKU WANANCHI WAKIHANGAISHWA NA WANYAMAPORI KACHELIBA.

Maafisa wa idara ya wanyamapori katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuwadhibiti wanyama pori ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi wa eneo la Kacheliba katika kaunti hii.

Msimamizi wa kaunti ndogo ya Kacheliba Daniel Okudoki amesema kwa muda sasa wanyama hao wamewahangaisha wakazi ambapo wamepata hasara kubwa baada ya mifugo wao kuliwa na wanyama hao na sasa mkazi mmoja amepoteza maisha kwa kushambuliwa na wanyama.

Aidha Okudoki aliwaka wabunge katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuwasilisha na kushinikiza kupasisha sheria itakayopelekea kuwafidia watu au familia za wanaoathiriwa na wanyama hao.

“Tunahangaishwa sana na wanyamapori maeneo haya. Wamekula mifugo wetu na sasa tunakadiria hasara kubwa. Hivi majuzi mtu mmoja amepoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba. Tunaomba tu maafisa wa KWS kuja kuwadhibiti wanyama hawa.” Alisema Okudoki.

Ni wito ambao ulikaririwa na wakazi wa eneo hilo ambao waliwalaumu pakubwa maafisa wa KWS kwa utepetevu, wakidai licha ya maafisa hao kupokea taarifa za uvamizi wa wanyama kwa wanadamu wamekuwa wakichukua muda kufika eneo la tukio.

“Maafisa wa KWS kaunti hii wamezembea sana katika majukumu yao. Kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukiripoti kuvamiwa na wanyama lakini wanachukua muda mrefu sana kufika eneo la tukio.” Walisema.