MAAFISA WA KPLC MJINI MAKUTANO KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WASHUTUMIWA NA WIZARA YA KAWI NCHINI.


Aliyekuwa gavana wa kwanza wa kaunti ya Pokot Magharibi ambaye kwa sasa ni katibu wa utawala katika wizara ya kawi Simon Kachapin ameshutumu maafisa wa KPLC mjini Makutano katika kaunti ya Pokot Magharibi kwa kutowajibika ipasavyo katika kazi ya kuunganisha nguvu za umeme katika maeneo mengi kwenye kaunti hii.
Amesema vikingi vingi vya nguvu ya umeme vimeanguka huku idara hiyo ikikosa kurekebisha kwa minajili ya kuwanufaisha wakazi wa kaunti hii.
Wakati huo huo amemsuta gavana wa Pokot Magharibi Prof. John Lonyangapuo kwa kupuuzilia mbali miradi ambayo ilianzishwa alipokuwa uongozini huku akimtaka Lonyangapuo kuhakikisha miradi hiyo inakamilishwa kutokana na hali kwamba ugavi wa mapato kutoka serikali kuu ulikuwa mdogo zaidi ukilinganishwa na wa muhula wa Lonyangapuo ambapo pesa ziliongezwa mara dufu kwa kaunti hiyo.