MAAFISA WA KDF WASUTWA KWA MADAI YA KUWAHANGAISHA WANANCHI LAMI NYEUSI.

Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wamewasuta maafisa wa usalama ambao wanaendesha oparesheni ya kuwakabili wahalifu ambao wamekuwa wakiendeleza wizi wa mifugo katika kaunti 6 za kaskazini mwa bonde la ufa, kufuatia jinsi ambavyo wanaendesha oparesheni hiyo.

Wakizungumza eneo la lami nyeusi ambapo mkazi mmoja alijeruhiwa mapema jumatano kwa kupigwa risasi na wahalifu hao, viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong walisema licha ya mkazi huyo kujeruhiwa na wahalifu, alikamatwa na maafisa wa KDF kwa kusingiziwa kuwa ni mmoja wa wanaoendeleza uhalifu eneo hilo.

Lochakapong amesema kwamba japo viongozi kaunti hiyo walikuwa wamejitolea kushirikiana na maafisa hao katika kuhakikisha kwamba wahalifu wanakabiliwa, itakuwa vigumu kuendeleza ushirikiano huo iwapo maafisa hao wataendelea na mtindo huu wa kuwahangaisha wakazi wasio na hatia.

“Mtazamo wangu kwa kikosi cha KDF ni tofauti sasa. Kwa sababu haiwezekani kwamba wanakuja kuleta usalama hapa na hao sasa ndio wanawahangaisha wananchi wenyewe. Kwa hivyo nasema kwamba sisi tungetaka kushirikiana na serikali kwa maswala ya amani lakini kama hivi ndivyo watafanya kazi, hatuwezi kubali.” Alisema Lochakapong.

Mwanaharakati wa amani Dkt. Charles Lochodo alisema kwamba kijana huyo alivamiwa na wahalifu na kupigwa risasi wakati akilisha mifugo, akiwataka maafisa wanaoendesha oparesheni hiyo kutekeleza majukumu yao ya kuwaandama wahalifu badala ya wakazi wanaoendesha shughuli zao.

“Kijana huyu alikuwa akilisha mifugo, alipokuja kuwanywesha maji ndipo akapatana na wakora ambao walimpiga risasi. Mimi nasema kwamba mtu yeyote ambaye anahusika kuvuruga amani anapasa kukabiliwa kulingana na sheria. Lakini wakazi ambao wanapenda amani wasije wakadhulumiwa wakati wanatekeleza shughuli zao za maisha.” Alisema Lochodo.

Wakazi wa eneo hilo wamelalamikia kuongezeka visa vya utovu wa usalama katika siku za hivi karibuni hali ambayo imetatiza shughuli zao za kila siku, ambapo kumeshuhudiwa mashambulizi mawili katika muda wa siku tatu zilizopita watu wawili wakiuliwa katika visa hivyo.

“Katika kipindi cha siku tatu mashambulizi mawili yametokea ambapo watu wawili wameuliwa katika visa tofauti huku mmoja akiendelea kuuguza majeraha. Hivyo tunataka serikali kutuokoa kwa sababu sasa watu wanaogopa kutekeleza shughuli zao za kila siku.” Walisema.