MAAFISA WA ELIMU POKOT MAGHARIBI WAENDESHA UKAGUZI SHULENI MASOMO YA GREDI YA SABA YAKIANZA RASMI.
Maafisa katika idara ya elimu na ile ya usalama kaunti ya pokot magharibi wamefanya ukaguzi katika baadhi ya shule kwenye kaunti hiyo wakati wanafunzi waliofanya mtihani wa gredi ya sita KIPSEA wakianza rasmi masomo ya gredi ya Saba.
Akiongoza maafisa wengine kutoka idara ya elimu kaunti hii ya Pokot magharibi, mkurugenzi wa tume ya huduma za walimu kaunti hiyo Benard Kimachas alisema kwamba kila shule ya sekondari ya msingi itapata mwalimu mmoja huku nafasi zilizosalia zikijazwa na walimu wa shule za msingi waliopokea mafunzo ya CBC.
“Tuna mipango ya kuleta walimu kuanzia wiki ijayo. Tutaanza kutuma mwalimu mmoja kwa kila shule. Tayari tumewasajili na kilichosalia ni kuwaandikia tu barua. Tutawatumia pia walimu wa shule za msingi ambao wametimu kufunza shule za upili ngazi ya chini kuwahudumia wanafunzi hawa.” Alisema Kimachas.
Kamishna wa kaunti ya pokot magharibi Apolo Okelo aliwahakikishia wazazi kwamba kila mwanafunzi wa gredi ya saba atatengewa shilingi alfu 15 ambazo zitakuwa zikitumwa kwenye akaunti ya shule huku akiwahimiza kutekeleza majukumu mengine ikiwemo kuwanunulia wanao sare na mahitaji mengine muhimu.
“Pesa ambazo zimetengwa kuhakikisha kwamba wanafunzi wa gredi ya saba wanaendelea na masomo zitatumwa kwa akaunti za shule. Kila mtoto atapata shilingi alfu 15000. Kazi ya mtoto itakuwa kusoma tu na kazi ya mzazi kununua sare na mahitaji mengine muhimu.” Alisema Apolo.
Kwa upande wake kamanda wa polisi kaunti hiyo Pater Katam aliwasihi wazazi kuwaruhusu wanao kusoma na kuafikia ndoto zao maishani, akiwaonya dhidi ya kuwaoza wanao wa kike kabla ya kumaliza masomo yao.
“Kila mtoto ana ndoto, na ni jukumu la mzazi kuhakikisha mtoto huyo anaafikia ndoto yake maishani. Kwa sasa, mzazi yeyote asitarajie kumwoza mtoto eti apate mali. Wacha huyo mtoto asome, atakuletea hiyo mali akishaafikia ndoto yake.” Alisema Katam.