MAAFISA WA ASTU WASHUTUMIWA KWA KUWAHANGAISHA WAKAZI WA KERINGET .

Na Benson Aswani

Wakazi wa eneo la Keringet kaunti ya Pokot magharibi wamewasuta maafisa wa usalama wa kitengo cha kukabiliana na wizi wa mifugo ASTU kwa kile wamedai kunyanyaswa na maafisa hao.
Wakiongozwa na Clemencia Mogere, wakazi hao walidai kwamba maafisa hao walivamia makazi yao kwa madai ya kuendeleza msako na kutekeleza uharibifu mkubwa huku wakiwahangaisha wakazi ambapo wengine wao wanaidai kupigwa na maafisa hao.
Walisema maafisa hao walitekeleza msako huo kinyume cha sheria kwani hawakuwa na kibali cha kuonyesha kwamba walifaa kuendesha shughuli hiyo eneo hilo.
“Maafisa wa ASTU walifika katika eneo hili na kuanza kuwahangaisha wananchi kwa madai ya kuendeleza msako. Walitupiga na kuharibu bidhaa zetu na hata kupora baadhi ya bidhaa. Wanaingia katika nyumba zetu hata bila ya kibali cha kuendesha msako huo.” Walisema.
Wakazi hao sasa wanawataka wakuu wa idara ya usalama wakiongozwa na waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kuangazia swala hilo kwani baadhi ya wakazi walipoteza bidhaa zao katika msako huo.
“Tunaomba waziri wa usalama Kithure Kindiki na inspekta wa polisi Japheth Koome kuingilia kati swala hili kwa sababu hawa maafisa wamepiga watu sana huku. Ikiwezekana wapelekwe huko mipakani mahali hakuna usalama wafanye kazi huko.” Walisema.
OCPD wa Kapenguria Joel Kirui alisema wamepokea taarifa hiyo na kwa sasa wanaendeleza uchunguzi, akiahidi kuhakikisha kwamba hatua zinachukuliwa dhidi ya maafisa watakaopatikana na makosa ya kuhusika dhuluma dhidi ya raia.
“Wananchi wa eneo hilo wameleta ripoti na sasa sisi tunaendelea na uchunguzi wetu. Tunawataka wanachi kuwa watulivu tunapoendeleza uchunguzi huu na tunawaahidi kwamba hatua zitachukuliwa dhidi ya maafisa ambao watapatikana kuhusika dhuluma dhidi ya wananchi.” Alisema Kirui.