MAAFISA WA AKIBA NPR POKOT MAGHARIBI WAANZA RASMI MAJUKUMU YAO.
Maafisa wa akiba NPR ambao waliteuliwa kuhudumu katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kushirikiana kikamilifu na maafisa wengine wa usalama ili kuhakikisha kwamba malengo ya kukabili utovu wa usalama hasa maeneo ya mipakani yanaafikiwa.
Akizungumza kwa niaba ya waziri wa maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki katika hafla ya kufuzu maafisa 205 wa NPR iliyofanyika eneo la Chesta wadi ya Lomut, mkurugenzi wa shughuli katika huduma ya polisi nchini Ranson lolmodoni aidha aliwahimiza maafisa hao kuwa na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao.
“Nawaeleza maafisa wa NPR ambao wamefuzu hii leo kwamba jambo la ushirikiano ni muhimu sana katika idara hii. Watapasa kushirikiana na wadau wote kutoka mashinani hadi kwenye ngazi ya kitaifa. Nidhamu pia ni muhimu zaidi.” Alisema Lolmodoni.
Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alipongeza mafunzo ya mwezi mmoja ambayo maafisa hao wamepokea akisema kwamba yatawasaidia pakubwa katika kutekeleza majukumu yao, akiahidi kushirikiana nao ili kuafikiwa malengo hitajika.
“Maafisa hawa wamepata mafunzo kamili. Hamna tofauti na waliopata mafunzo yao huko Kiganjo na Embakasi hivyo nawapongeza kwa kustahimili mafunzo haya ya mwezi mmoja. Mimi kama gavana naahidi kushirikiana kikamilifu na maafisa hawa ili kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa.” Alisema Kachapin.
Wakuu wa usalama wakiongozwa na kamanda wa polisi kaunti hiyo Peter Katam waliwahakikishia wakazi kwamba maafisa hao wamepewa mafunzo ya kutosha na kukabidhiwa vifaa ambavyo watatumia kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Hawa maafisa wamepata mafunzo yanayostahili na pia wamepewa vifaa hitajika, na hivyo wanaanza mara moja majukumu yao katika sehemu ambako watatumwa.” Alisema Katam.