MAAFISA TRANS NZOIA WAONYWA DHIDI YA KUJIHUSISHA NA KAMPENI ZA UCHAGUZI.
Maafisa wa serikali ya kaunti ya Trans nzoia wametakiwa kukoma kujihusisha na kampeni za uridhi wa gavana Patrick Khaemba na badala yake kuwahudumia wakazi wakati wakisubiri kumpigia kura mgombea yeyote watakayempendelea katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.
Akizungumza katika kikao na wafanyikazi wote wa kaunti hiyo takriban majuma matatu kabla ya kukamilika hatamu ya uongozi wa mihula miwili, Khaemba amewataka maafisa hao kutojipaka tope la kampeni za uridhi wake akisema huenda hatua hiyo ikaleta uhasama kati yao na baadhi ya wanasiasa hali ambayo huenda ikahatarisha kazi zao.
Wakati uo huo Khaemba amejitenga na madai kuwa anamuunga mkono mgombea ugavana kaunti hiyo kupitia chama cha Ford Kenya Dkt Chris Wamalwa kufuatia uamuzi wake wa kufanya kazi na naibu rais William Ruto ambaye anamuunga Wamalwa chini ya muungano wa Kenya kwanza.
Ametumia fursa hiyo kutetea rekodi yake ya maendeleo katika kipindi cha mihula miwili aliyohudumu kama gavana wa kaunti hiyo ya Trans nzoia.