LOTEE: RAIS WILLIAM RUTO ANA MAONO MAZURI KWA AJILI YA TAIFA LA KENYA.
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuunga mkono mapendekezo ya rais William Ruto kuongeza ushuru nchini ili kufanikisha miradi ya serikali.
Wa hivi punge kuzungumzia swala hilo ni mbunge wa Kacheliba Titus Lotee ambaye alisema kwamba rais Ruto ana maono mazuri ya kuhakikisha kwamba serikali yake haiongezei mkenya mzigo kwa kuendelea kukopa kutoka mataifa ya nje.
Aidha Lotee aliwasuta wanaopinga mpango huo wa serikali kwa kile alidai kuingiza siasa kwa maswala yanayonuiwa kumfaidi mwananchi wa kawaida, huku akiwahakikishia wakazi kwamba ni wafanyikazi wanaolipwa na serikali tu watakaotozwa ushuru huo.
“Rais ana maono kwa ajili ya taifa hili na ndio maana amekuja na mswada wa fedha wa mwaka 2023 ili kuwasaidia wakenya kutoka katika hali ya kukopa madeni kila mara kutoka mataifa ya nje. Ila sasa swala hili limeingizwa siasa ilhali watakaotozwa asilimia tatu ya mshahara wao ni watu wanaolipwa na serikali.” Alisema Lotee.
Lotee alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kushirikiana na serikali ili kuhakikisha kwamba maisha ya mwananchi wa kawaida yanaimarika na kupuuza dhana kwamba mikakati hiyo ya rais inalenga kuwanyanyasa wananchi.
“Sisi tunaomba kwamba jinsi ambavyo rais amekuwa na maono haya ya kuondoa taifa katika madeni, tushirikiane naye katika kuendeleza taifa mbele. Tusihadaike na wale ambao wanasema kwamba rais analenga kuwanyanyasa wananchi. Rais hana nia hiyo.” Alisema.