Lotee akemea hazina ya taifa kwa kuchelewesha fedha za CDF

Mbunge wa kacheliba akizundua Basari,Picha/Joseph Lochele
Na Emmanuel Oyasi,
Mbunge wa Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi Titus Lotee amezindua basari ya kima cha shilingi 60,000,000, katika hafla ambayo iliandaliwa alhamisi tarehe 15 mwezi Mei.
Hili ni ongezeko la shilingi 15,000,000 kutoka shilingi 45,000,000 ambazo alitengea basari mwaka jana.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyoandaliwa katika shule ya upili ya Kodich eneo bunge la Kacheliba, Lotee alilalamikia kucheleweshwa fedha za CDF hatua ambayo alisema imechangia kuathirika pakubwa shughuli mbali mbali ikiwemo swala la masomo shuleni.
Lotee aliisuta hazina ya kitaifa kwa kile alidai kuzembea katika majukumu ya kuhakikisha fedha za maendeleo zinafikia wabunge kwa wakati.
“Mwaka huu tumepata changamoto sana, kwamba mwezi Mei ndio tunazindua basari hali wanafunzi wetu walienda shuleni mwezi januari. Hii ina maan kwamba wale wanaoshughulikia fedha za CDF katika hazina ya kitaifa wamechukua mkondo usiofaa,” alisema Lotee.
Wakati uo huo Lotee alitofautiana na pendekezo la kuondolewa hazina ya CDF mikononi mwa wabunge, akisema kwamba idadi kubwa ya wakenya wanaunga mkono kuendelea kuwepo hazina hiyo kutokana na manufaa yake nchini.
“Kuna wale ambao wanasema CDF iondolewe. Lakini katika vikao ambavyo tumekuwa navyo na wananchi, wengi wao wanasema CDF iendelee kwa sababu imekuwa na manufaa mengi sana,” alisema Lotee.
Ni hatua ambayo ilipongezwa na wakuu wa shule katika eneo bunge hilo wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Kodich Mark Losia ambaye alisema itafanikisha shughuli ambazo zilikuwa zimekwama shuleni na kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo bila ya changamoto ya karo.
“Tunashukuru sana kwa uzinduzi wa basari. Hii itasaidia kuhakikisha kwamba wanafunzi wanasalia shuleni na hivyo kuendeleza shughuli mbali mbali za masomo ambazo zilikuwa zimekwama,” alisema Losia.