LOPETAKOU: AMANI ITAAFIKIWA KASKAZINI MWA BONDE LA UFA IWAPO WAKAZI WATAKUMBATIA ELIMU NA SHUGHULI ZA MAENDELEO.
Hali ya usalama itarejea tu katika kaunti za kaskazini mwa bonde la ufa iwapo wakazi wa maeneo haya watakubali kuasi hali yao ya maisha na kukumbatia mabadiliko.
Haya ni kwa mujibu wa William Lopetakou anayehusika na maswala ya utamaduni kaunti ya Pokot magharibi, ambaye alisema kaunti hizi zitaafikia amani iwapo wakazi watakumbatia elimu na kuasi hulka zilizopitwa na wakati kama vile wizi wa mifugo ambao ndio chanzo kikuu cha utovu wa usalama maeneo haya.
Lopetakou alisema iwapo wakazi wa maeneo haya wataendelea kushikilia hulka hii ya tangu jadi, huenda oparesheni ya usalama inayoendelezwa na maafisa wa polisi kwa ushirikiano na wenzao wa KDF ikakosa kuzaa matunda yanayotarajiwa.
“Amani itapatikana tu kaskazini mwa bonde la ufa iwapo wakazi watageuza mawazo yao na kuasi wizi wa mifugo. Iwapo wakazi watakumbatia elimu na kujihusisha na shughuli za kuwapa kipato cha kila siku, hapo ndipo tutapata amani.” Alisema Lopetakou.
Wakati uo huo Lopetakou alilaumu matamshi ya kiholela yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa katika maeneo haya na kuyataja kuwa uchochezi ambao unazidisha uhasama miongoni mwa wakazi.
“Kuna viongozi wa kisiasa ambao wanatoa matamshi kiholela na ambayo yanachochea wakazi kujihusisha na vitendo vya uvamizi. Ni maombi yetu kwamba viongozi wa kisiasa wafahamu umuhimu wa wananchi kuishi kwa amani ili hata nasi tupate maendeleo.” Alisema.