LONYANGAPUO: SULUHU KWA TATIZO LA NJAA KAUNTI HII NI KWA KILA MMOJA KWENDA SHAMBANI.

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Pokot magharibi John Lonyangapuo ameelezea haja ya kuwekeza pakubwa katika kilimo ili kukabili tatizo la njaa ambalo limekuwa kizungumkuti kila wakati wa kiangazi katika kaunti hiyo.

Lonyangapuo ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi katika shirika la maji na maendeleo kaskazini mwa bonde la ufa alisisitiza kwamba kikombozi cha kaunti hiyo na taifa la Kenya kwa jumla kutokana na tatizo la njaa ni kwa kila mmoja kuelekea shambani licha ya hadhi yake katika jamii.

“Taifa la Kenya litaokoka tu iwapo kila mmoja atakumbatia kilimo. Iwapo kila mmoja ataondoka katika eneo lake la starehe na kwenda shambani, hapo ndipo tutaweza kukabili tatizo la njaa ambalo limekuwa likishuhudiwa kaunti hii na maeneo mengine nchini kila wakati wa ukame.” Alisema Lonyangapuo.

Aidha Lonyangapuo alizitaka serikali za kaunti kuweka kipau mbele kwa wataalam wa kilimo ili kusaidia katika kuimarisha shughuli za kilimo ambacho kimetajwa kuwa ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hili.

“Serikali zote hasa za kaunti zinapasa kulipa kipau mbele swala la kuajiri wataalam wa kilimo ambao wataweza kusaidia katika kuimarisha kilimo cha mimea na mifugo kwa jumla, kwa kutoa ushauri unaopasa kuhusiana na maswala yanayohusu kilimo.” Alisema.