‘LONYANGAPUO HANA UMAARUFU TENA POKOT MAGHARIBI’, ASEMA ATUDONYANG.


Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi John Lonyangapuo alipoteza umaarufu wake wa kisiasa katika kaunti hii baada yake kujiondoa katika chama cha KANU na kubuni chama cha KUP kinachotajwa kuwa cha kikabila.
Haya ni kwa mujibu wa naibu gavana kaunti hii Nicholas Atudonyang ambaye pia ametangaza nia ya kugombea kiti cha ugavana kaunti hii akisema kuwa hatua yake kugombea kiti cha ugavana imetokana na shinikizo kutoka kwa wananchi ambao amedai kuwa hawataki kujihusisha na vyama vya kikabila huku akisisitiza wataendelea kuunga mkono mrengo wa azimio la umoja.
Wakati uo huo Atudonyang amekariri kuwa gavana Lonyangapuo hataweza kushinda uchaguzi mkuu ujao na ni kufuatia hofu hiyo ambapo aliamua kushirikiana na muungano wa azimio la umoja ili kujipatia nafasi katika serikali kuu iwapo atapoteza kiti cha ugavana.
Wakati uo huo seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio ametetea hatua ya Atudonyang kutofanya kazi na gavana Lonyangapuo licha ya kuwa naibu gavana akisema kuwa hatua hii inatokana na tabia ya gavana Lonyangapuo kutotoa ushirikiano mwema kwa watu anaofanya nao kazi.