LONYANGAPUO AWASUTA VIONGOZI WANAOENDELEZA KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2027.
Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Pokot magharibi John Lonyangapuo amelalamikia hatua ya baadhi ya viongozi ambao alisema kwamba wameanza kuendeleza kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 mwaka mmoja tu tangu taifa kuandaa uchaguzi mkuu.
Akizungumza na wanahabari Lonyangapuo alisema kwamba viongozi hao wamesahau kazi ya kuwahudumia wananchi ambao waliwachagua katika nafasi hizo na kuanza siasa za uchaguzi mkuu ujao akiwataka kujiuzulu na kuwapa nafasi viongozi ambao wako tayari kutoa huduma kwa wananchi.
“Ni mwaka mmoja tu tangu tuwe na uchaguzi na ni wakati ambapo viongozi ambao walichaguliwa wanapasa kuwa wamezingatia sana huduma kwa wananchi. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba baadhi ya viongozi sasa wameanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao badala ya kuwahudumia wakazi.” Alisema Lonyangapuo.
Wakati uo huo Lonyangapuo aliwasuta baadhi ya viongozi ambao wanamezea mate kiti cha ugavana miaka minne kabla ya uchaguzi mkuu ujao, akidai azma yao kuwania kiti hicho si huduma kwa wananchi bali wanaongozwa na kile alitaja kuwa tamaa ya kupora mali ya umma.
“Halafu kuna wengine wameanza kumezea mate kiti cha ugavana. Hawa ni wale wanadhani kwamba ukiwa gavana sasa una nafasi ya kuiba pesa za umma. Lengo lao si kuwahudumia wananchi bali ni kupata nafasi ya kupora mali.” Alisema.