LONYANGAPUO ASUTWA KWA KUTOCHUKUA HATUA KUKABILI BAA LA NJAA POKOT MAGHARIBI.
Mbunge wa kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto amemsuta gavana wa kaunti hii John Lonyangapuo kwa kile amedai kutowajibika katika kushughulikia baa la njaa ambalo linashuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya kaunti hii.
Moroto ameelezea kushangazwa na hali kuwa hadi kufikia sasa serikali ya kaunti chini ya uongozi wa gavana John Lonyangapuo haijachukua hatua yoyote licha ya kuwepo hazina ya kushughulikia majanga kwa kila kaunti.
Amesema kuwa wabunge katika bunga la kaunti hii walipasisha shilingi milioni 50 za kununua chakula kwa ajili ya wakazi wanaokabiliwa na makali ya njaa kabla ya kuahirishwa vikao vya bunge hilo, ila chakula hicho hakijanunuliwa kufikia sasa na badala yake Lonyangapuo kutumia msaada unaotolewa na serikali kuu kujipigia debe.
Moroto ametumia fursa hiyo kumshukuru rais Uhuru Kenyatta na serikali yake kwa kutuma chakula cha msaada kwa ajili ya wakazi wa kaunti hii akisema kuwa idadi kubwa ya wakazi wa kaunti hii inakabiliwa na makali ya njaa.