LONYANGAPUO ASUTWA KWA KUKITHIRI UFISADI KWENYE SERIKALI YAKE.


Mwaniaji ugavana katika kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendeleza shutuma dhidi ya gavana wa sasa ambaye pia anatetea kiti hicho kupitia chama cha KUP John Lonyangapuo kwa madai ya kukithiri uporaji fedha za umma katika serikali yake.
Kachapin ambaye anawania kiti hicho kupitia chama cha UDA amedai kuwa matumizi mabaya ya fedha za umma na serikali ya gavana Lonyangapuo yamepelekea kaunti hii kusalia nyuma kimandeleo licha ya kutengewa kiwango kikubwa cha fedha ikilinganishwa na awamu yake alipohudumu kama gavana wa kwanza wa kaunti hii.
Kachapin sasa anamtaka Lonyangapuo kujitokeza wazi wazi na kukanusha taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini ambalo lilimworodhesha miongoni mwa magavana 10 waliofuja fedha zinazotengewa kaunti zao iwapo anadai hakuhusika uovu huo.
Wakati uo huo Kachapin amewataka wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kuwa makini katika uchaguzi mkuu wa tarehe 9 mwezi huu wa agosti na kumchagua ili aendeleze miradi aliyoanzisha na kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika katika njia inayofaa.