LONYANGAPUO ASUTA UDA KWA MADAI YA KUENEZA PROPAGANDA KUHUSU MGOMBEA MWENZA.

Wafuasi wa chama cha KUP katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kutokuwa na hofu kuhusiana na hatima ya mgombea mwenza wa mgombea wa ugavana wa kaunti kupitia chama hicho gavana John Lonyangapuo.
Akizungumza na wanahabari Lonyangapuo amesema kuwa wagombea wenza wanaruhusiwa kisheria kuendelea na majukumu yao hadi wakati ambapo wanachaguliwa kuwa wagombea wenza ndipo wataweza kujiuzulu nyadhifa zao serikalini.
Wakati uo huo Lonyangapuo amewashutumu viongozi wa chama cha UDA katika kaunti hii kwa kile amedai kuwa ndio wanaoeneza propaganda kuwa amemteua mgombea mwenza ambaye hakuwa amejiuzulu wadhifa wake serikalini.
Aidha Lonyangapuo amebainisha majina ya mgombea mwenza wake kutokana na hali kuwa huenda yakaleta mkanganyiko na yale ya mgombea wa ugavana kaunti hii kupitia chama cha UDA Simon Kachapin akiwataka wafuasi wake kuwa makini na kutochanganyikiwa wakati wa upigaji kura.