LONYANGAPUO AKOSOLEWA KWA HATUA YAKE YA HIVI PUNDE KUWAAJIRI MAAFISA ZAIDI.

Hata licha ya gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi John Lonyangapuo kuonya dhidi ya kuingizwa kile alichotaja kuwa siasa katika shughuli ya hivi punde kuwaajiri maafisa zaidi katika serikali yake, baadhi ya viongozi katika kaunti hii wamekosoa hatua hiyo.
Wakiongozwa na seneta Samwel Poghisio, viongozi hao wamesema gavana Lonyangapuo hakustahili kuchukua hatua hiyo hasa ikizingatiwa kuwa muhula wake wa kwanza katika uongozi wa kaunti hii unaelekea kukamilika.
Poghisio amedai kuwa huenda Gavana Lonyangapuo anafahamu kuwa hatorejea tena uongozini na alichukua hatua hiyo ya kuwazawidi washirika wake ili kumzuia mrithi wake dhidi ya kuwaajiri maafisa zaidi katika serikali ijayo.
Poghisio amesema kuwa uchumi wa kaunti hii kwa sasa hauruhusu kuajiriwa maafisa zaidi ya wale waliopo kwa sasa huku akiahidi kuchukuliwa hatua dhidi ya swala hili na gavana ambaye atachukua usukani baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.