LOCHAKAPONG ASUTA AFISI YA REREC KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI KWA KUKUBALI KUTUMIKA KISIASA.
Mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter lochakapong sasa anataka afisi ya shirika la usambazaji umeme maeneo ya mashinani Rural Electrification and Renewable Energy Corporation (REREC) kufanyiwa uchunguzi kwa kile amesema kwamba kutumika kisiasa.
Katika kikao na wanahabari, Lochakapong alisema kwamba kaimu afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo anatumika vibaya na baadhi ya wanasiasa kusambaza umeme katika maeneo yao huku maeneo mengine yakitengwa katika shughuli hiyo.
Lochakapong alidai kwamba afisa huyo anaegemea zaidi maeneo bunge ya viongozi waliochaguliwa katika mrengo wa upinzani akisema kama viongozi kamwe hawatakubali hali hiyo kuendelea.
“Kaimu afisa mkuu wa REREC amekubali afisi yake kutumika kisiasa. Anatumiwa na viongozi ambao walichaguliwa kupitia mrengo wa upinzani katika shughuli ya kusambaza umeme katika kaunti hii ya Pokot magharibi. Sisi hatuwezi kukubali hiyo tabia ya kuruhusu afisi yake kutumika vibaya na upinzani.” Alisema Lochakapong.
Lochakapong alimtaka afisa huyo kutekeleza majukumu yake kulingana na sheria kwa kuheshimu kila kiongozi ambaye alichaguliwa, na kwa kuzingatia uwazi ikizingatiwa anahudumu katika afisi ya umma.
“Afisa huyu anapasa kufahamu kwamba anahudumu katika afisi ya serikali na hafai kuruhusu afisi hiyo kudhibitiwa na wanasiasa. Anapasa kuheshimu viongozi wengine na kufanya majukumu yake kwa mujibu wa sheria ili tufanye kazi pamoja.” Alisema.