LOCHAKAPONG AAHIDI KURAHISISHA SHUGHULI ZA WAKAZI WA SIGOR KUPITIA UKARABATI WA BARABARA.
Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong amesema kwamba atahakikisha barabara zote katika eneo bunge lake ambazo haziko katika hali nzuri zinakarabatiwa ili kurahisisha shughuli za uchukuzi kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa kuzindua barabara ya kuelekea shule ya Topeyeny, Lochakapong alisema kwamba shughuli nyingi eneo hilo zilikwama kutokana na ubovu wa barabara, hatua iliyomlazimu kuikarabati kwa kupitia fedha za maendeleo kwa maeneo bunge CDF.
Aidha Lochakapong alisema shughuli za kibiashara sasa zitaimarika baada ya kukarabatiwa barabara hiyo kwani sasa wakulima watakuwa na nafasi nzuri ya kufikisha bidhaa zao sokoni kwa wakati kinyume na ilivyokuwa wali.
“Tunamshukuru Mungu kwa sababu sehemu hiyo ilikuwa imefungwa kwa muda na hivyo haingeweza kufikika kutokana na ubovu wa barabara. Lakini sasa tunafurahi kwa kujengwa barabara hii na sasa wakazi wanaweza kufanya shughuli zao bila tatizo ikiwemo kufikisha bidhaa zao sokoni.” Alisema Lochakapong.
Wakati uo huo Lochakapong alisema shughuli katika shule ya Topeyeny zitaendelea inavyopasa kwani sasa itaweza kufikika kwa urahisi.
“Hii shule ambayo inaitwa Topeyeny haikuwa inafikika kwa sababu hakukuwa na barabara, lakini sasa walimu watapata urahisi wa kufika shuleni humo. Itakuwa rahisi pia kupeleka huduma mbali mbali katika shule hiyo ikiwemo chakula na vifaa vya ujenzi.” Alisema.